Matukio ya Mwezi wa Ramadhani-Vita vya Badr-2


Katika sehemu hii ya mwisho, tunaelezea hali ilivyokuwa vitani hadi Waislamu kupata ushindi.

Kuelekea Vitani

Kulikuwa na kazi kubwa ya kubadilisha mawazo ya haraka kutoka kwenye kuvamia msafara na kupata mali bila ya taabu na mambo kubadilika kuelekea kwenye mapambano ambayo yana vishindo ndani yake ijapokuwa Allah alikwisha waahidi kuwa watapata moja kati ya mambo mawili kuuteka msafara au ushindi katika vita. Allah kwa upande aliwapangia vita ili kuwafedhehesha Makafiri na kuisimamisha dini yake.

Kabla ya Mtume SAW kuchukua hatua yoyote ile kuelekea vitani, akasimama na kuanza kutaka ushauri kutoka kwa Masahaba zake kuhusu kuingia vitani au hawatakuwa nae kwa sababu walilolikusudia wamelikosa? Sahaba wa mwanzo kumuunga mkono alikuwa Syd Abubakar aliotamka kinaga ubaga kuwa atakuwa na Mtume SAW kihali umali kisha akfwatia Syd Umar bin Khatab , kisha akasimama Sahaba Mikdad bin Amru akasema:
“Ewe mjumbe wa Mwenye enzi Mungu, fanya lile alilokuamrisha Mola wako (yaani vita) nasi tupo pamoja nawewe wala hatutakuambia kama bani Israili walipomuambia Nabii Mussa,-Nenda wewe na Mola wako ukapigane sisi tupo hapa tunakusubiri, lakini sisi tunakuambia, Nenda na Mola wako nasi tupo pamoja katika mapambano”.

Mtume SAW akamuombea dua Mikidad nakuwataka ushauri Masahaba kwa kusema “Nishaurini enyi watu wangu?” Mtume baada ya kuufahamu msimamo wa Muhajirina alitaka kuujuwa msimamo wa Maansar kwasababu idadi yao ilikuwa ni kubwa kuliko Waislamu, akasimama Sahaba Saad bin Muaadh (kiongozi wa watu wa Madina) akasema:
“Kama kwamba unatukusudia sisi tukushauri ewe mjumbe wa Allah?”
Mtume SAW akajibu “ndio” Saad akasema “Sisi tumekuamini na tumeyasadiki uliyokuja nayo na tumeshuhudia kuwa uliyokuja nayo ni ya haki, aidha tulikupa ahadi, sisi tunasikiliza amri yako na tupo pamoja nawewe fanya ulitakalo wala hatuchukizwi kupambana na maadui zetu.”

Hapo ndipo Mtume akatoa amri ya mapambano na akasema “Nendeni na kubashirieni ushindi Mwenye enzi Mungu ameniahidi moja kati ya makundi mawili, kuvamia msafara au vita.”
Siku iliofwata akawatangazia kuwa ni siku ya vita. Masahaba walilala usiku wa kuamkia siku ya vita usingizi wa raha wa kuondoa machofu yote. Hii ilikuwa neema kutoka kwa Mola wao ili siku ya mapambano wawe wachangamfu, tofauti wangalikuwa kama kawaida wa mwanadamu anapofikwa na jambo muhimu tena zito basi huwa usiku kucha analiwaza na kulifikiri lakini Allah aliwapa Waislamu usingizi mwanana ikiwa ni ishara ya ushindi.

Walipoamka wengine walihitaji maji ya kukoga nao hawakuwa na maji, Allah SW akawateremshia mvua ambayo iliwasaidia kwa mengi ikiwemo kuwatoharisha, kuwatoa wasiwasi wa Shetani kwa kuwa na shaka juu ya walifanyalo, nakuweza kuwapa thika juu ya walifanyalo kuwa Allah yupo pamoja nao. Kutokana na hayo, aliwapa wepesi wa kutembea jangwani ikiwa ardhi imeshikamana na mchanga.
“Mlipo kuwa mkimuomba msaada Mola wenu Mlezi, naye akakujibuni kuwa: Kwa yakini Mimi nitakusaidieni kwa Malaika elfu wanao fuatana mfululizo.” (8:11)

Upande wao makafiri hali ilikuwa vyengine. Upande wao ulijaa tope na kuwafanya kutoweza kutembea vizuri.
Mtume akawaamrisha masahaba waelekee karibu na maji ya Badri walipofika akauliza Sahaba Habbab bin Mundhir, akiwa alikuwa mjuzi wa mambo ya kivita, akanena “Ewe Mjumbe wa Mwenye enzi Mungu umepewa wahyi tufikie hapa au ni mbinu za kivita tu ?”. Mtume SAW akajibu kuwa zilikuwa ni mbinu za kivuta tu. Sahaba Habab akasema “Basi mimi nashauri tushuke mpaka kwenye maji yenyewe tukifanya hivyo tutapata kunywa maji, kisha tutatengeneza hodhi letu kisha tutafukia madimbwi yote ili wakija Makafiri wasipate maji ya kunywa. Tutapata kuwapiga kwa wepesi wakiwa na kiu.”
Mtume SAW akaungaa mkono rai hii, wakaelekea hadi sehemu ya maji kisha Sahaba Saad bin Muadh akashauri ajengewe Mtume kijibanda cha kukaa kwa mapumziko na ushindi utapopatikana atakuwa amehifadhika. Mtume SAW akawafiki pia rai hii pakajengwa na akawa Sahaaba Abubakar yupo mlangoni na wengine wapo pembezoni wote wakiwa wanamlinda Mtume SAW asije akadhuriwa katika vita.

Maakafiri waalipofikaa sehemu hiyo na kukutana na Waislamu ana kwa ana wakiwa na kiu na maji hawana hawakuweza kustahamili kuna baadhi yao walikwenda kuomba maji kwa Waislamu na kutokana na mafunzo ya Kiislamu waliwagawia maji wakanywa na kila aliyekunywa aliuliwa katika vita hivi isipokuwa mmoja tu. Hapa msomaji atatakiwa afahamu kuwa walipewa maji wakanywa kiu ikawaondoka kisha kwenye vita ndio wakauliwa.

Baadhi ya makafiri walipowaona Waislamu idadi yao na walivyokuwa wapo imara wakaanza kubabaika na kutaka kurudi Makka na walikhofu wasije wakawauwa ndugu zao ambao ni Waislamu wa Makka kisha wakaja kujuta badae. Abu Jahaal kiongozi wa Makafiri akawagomba na kuwatia pampu mpaka wakaamua kuingia vitani na kusmea potelea mbali.

Kuanza kwa Vita

Kabla ya kuanza vita, Mtume SAW akalipanga jeshi lake kisha akawasomea hotuba na kuwakataza kuwauwa badhi ya makafiri na akawataja kwa majina akiwemo bwana Abbas ami yake Mtume SAW na hii inatokana na kujuwa kwake Mtume kuwa hao wametoka na kufwata rubaa kwa kuwaonea haya makafiri lakini hawakuwa tayari kwenda kupigana na Waislamu.

Mtume akawambia “mwenye kuuliwa leo katika vita hivi hali yakuwa amepigana kwa kutaraji thawabu, basi ataingiaa peponi.”

Maneno hayo yaliwashajiisha Waislamu hapo tena vita vikaanza kama kawaida ya Warabu katika mapambano ya siku hizo, vita huanza kwa kupambana mmoja mmoja kutoka kila upande kisha ndio vita hupamba moto.

Upande wa Makafiri walitoka wapiganaji 3 akiwa Utbah bin Rabiah na ndugu yake aitwaye Shaaiba bin Rabiah na mwanawe aitwae Walid bin Utbah bin Rabiaah. Kwa upande wa Waislamu Mtume SAW akawachagua Hamza bin Abdul Muttalib ami yake Mtume SAW, kisha Syd Ali bin Abi Talib mtoto wa ami yake Mtume na wa mwisho alikuwa ni Ubaidah bin Harith ikiwa wote hao watu wa Makka na wanakutana kiukoo.

Mtume aliwachaguwa hawa baada ya kuwarejesha Maansari waliojitokeza ili mapambano yaanze kwa ndugu kwa ndugu. Hamza akamuuwa Shaibaah wakati Syd Ali akamuua Waliyd ama Ubaaydah alipambana na Harith mapambano yao yalikuwa makali na Ubaydah alijeruhiwa vibaya ndipo Syd Hamza akamaliza Harith na kumchukuwa Ubaydah hadi kwa Waislamu. Makafiri baada ya kuona wameshindwa njia hii, wakaamua kuanza vita kwa pamoja na Mtume alikuwa ashawaandaa watu wake namna ya kupambana akiwa amewaweka wapiganaji kwa safu, wapiganaji wa mishale wa mikuki, mbinu hii ilifana na ikaweza kuleta ushindi wa haraka.

Matokeo Bada ya Vita

Vita hivi waliuliwa viongozi wengi wa makafiri ikawa idadi ya waliouliwa katika makafiri ni 70 na mateka wakawa 70, upande wa Waislamu waliuliwa 14 kati ya hao 6 wakiwa Muhajirina na 4 wakiwa katika Maansari.

Kwisha kwa vita Mtume SAW akamtuma mjumbe kwenda kupeleka Madina habari za ushindi, kisha akawakusanya mateka na akawauliza Masahaba zake nini awafanye kwa kuwa Wahyi haukuteremka wakati huo. Syd Abubakar akatoa rai kuchukuliwe fidia kisha waachwe huru kwani huwenda siku za mbele wakasilimu, Syd Umar kwa upande wake alipendekeza wakatwe vichwa wote asibaki mtu kaati yao. Mtume SAW akachukua rai ya Syd Abubakar na akawataka wale wenye uwezo wajikomboe na wale wasio kuwa na fedha wenye kujuwa kusoma na kuandika wawasomeshe Waislamu mpaka watapohitumu kusoma na kuandika ndio kitakuwa kikombozi chao chakuwa huru.

Baada ya muda ikaja aya ambayo iliwafiki rai ya Syd Umar. Hata hivyo, rai ya Umar ndiyo ilikuwa sahihi iliteremka baadae badae aya kufahamisha Mtume kuwa ikuwa asichukuwe fidia bali alikuwa awauwe.


“Haimfalii Nabii yeyote kuwa na mateka mpaka awe ameshinda barabara katika nchi. Mnataka vitu vya dunia, na Mwenyezi Mungu anataka Akhera. Na Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu Mwenye hikima.” (8:67)

“Lau isingeli kuwa hukumu iliyo kwisha tangulia kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ingeli kupateni adhabu kubwa kwa vile mlivyo chukua.” (8:68)

“Basi kuleni katika mlivyo teka, ni halali na vizuri, na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.” (8:69)

Mafunzo Yanayopatikana

Mafunzo ynayopatikana katika vita hivi ni mengi mno baadhi yao ni kama ifwatavyo: Kiongozi kutojiamulia tu kujiona kuwa ni kiongozi, lakini kiongozi hutakiwa kuchukua ushauri kwa anawaongoza na kama atapewa ushauri wa jambo hata kama hakuuliza yeye basi angalie kama kuna maslahi, hana budi kuliwafiki. Na Mtume SAW sio alikubali rai ya Masahaba kwenye vita hivi tu, bali ilikuwa ndio khulka yake kushauriana na anaowaongoza. Alizijali rai za masahaba wake. Kuchukua rai za mtu anawaongoza ni kufata nyao za Mtume SAW.

Funzo jengine ni kusimamisha dini kwa kujitolea. Haya tunayaona namna Waislamu walivyokuwa imara kutomuacha kiongozi wao peke yake, bali walikuwa nae bega kwa bega kuhakikisha wanainusuru dini ya Mola wao mbali ya uchache wao na kutokuwa na silaha za kutosha. Yote haya waliyasahau na kuangalia moja tu, la kumnusuru Mtume SAW na makafiri.
Waislamu wa wakati huu hatunae Mtume SAW, lakini moja ya njia ya kuinusuru dini hii na kumnusuru Mtume SAW na maadui ni kufuata maarisho yake na miongozo yake katika harakati zetu zote.

Funzo jengine ni kuwa ushindi unatokana na imani, ndio ilivyokuwa katika vita hivi. Imani thabiti ya Masahaba ilikuwa kubwa kwa Mola wao kuwa atawanusuru pia kuwa kwao tayari kutii amri za Mtume SAW. Kwa kufanya hivyo ndio nusura ikawafika. Laiti wangelikuwa waasi, basi wasingeliupata ushindi kama huu kwani siri ya ushindi ni kutakasa nyoyo na kila machafu na kuwa na imani thabiti.

Aidha, kuna funzo ambalo Mtume SAW alilolifanya ambalo kwa miaka ya sasa lipo kinyume kabisa. Katika vita vya mmoja mmoja, Mtume SAW aliwatoa wale ambao wa ukoo wake na kuhakikisha ndio watakao anza mapambano. Leo kila alio wako utamtaka awe nyuma na kuwasukuma mbele wale waliokuwa sio wako.

Vita vya Badr ni chuo ambacho kimejaa mafunzo pomoni. Ilivyokuwa vimepiganwa katika mwezi hu wa Ramadhani, tujitahidi kujifunza na kuelewa falsafa yake na kutoona kuwa Waislamu katika dunia hii tunaonewa, wakati idadi yetu ipo kubwa kinyume waliopigana vita vya Badr walikuwa wachache wa idadi na wingi wa imani. Tuliopo sasa ni wengi wa idadi na wachache wa imani.
Share on Google Plus

About mfaume

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment