soma hapa hukumu waliopewa waislamu waliokamatwa Morogoro


‘Magaidi’ waliokamatwa Morogoro.
Wakiwa mbali na nyumbani kwao na miaka saba (7) sasa toka waanze kutumikia kifungo, mara moja moja Shain, Tony na Eljvir hupata fursa ya kuwasiliana na wazazi wao ambao sasa ni wazee.
“Inshaallah Mungu akipenda tutaonana tena.” Ni maneno ya faraja na matumaini ambayo watoto hao huwa wanamalizia mazungumzo yao kila wanapopata fursa ya kuongea na wazazi wao kwa simu.
“Nawapenda watoto wangu, Alhamdulillah bado tunaishi na mnatupa nguvu na faraja mnapotupigia tukawasikia mkiwa na matumaini juu ya Rehma na Nusra ya Allah. Hakuna wa kutegemewa ila yeye pekee Allah SWT.”
Ni maneno ya baba yao akionekana akiongea katika mkanda wa video huku machozi yakimtiririka. (Tazama Video, Duka Brothers ‘Entrapped’ juu ya mkasa huo.)
Wakati huo huo, huko nyumbani, hali inazidi kuwa mbaya kwa Mzee Firiki Duka na mkewe Bi Lata. Kijana wao Tony amewaachia mke na wajukuu watano ambao inabidi wawaangalie. Kijana wao mdogo Burim, amelazimika kaucha shule ili ahangaike mtaani angalau wapate kula.
Akiongea kwa masikitiko, lakini mithili ya machozi ya mamba, mtu aliyesababisha vijana hawa wa familia moja kufungwa, Mahmoud Omar akihojiwa na mwandishi mmoja anayetafiti juu ya kesi ya vijana hawa anasema, hata yeye anasikitika na hajui ni kwa nini vijana hao wamefungwa kwani walikuwa Waislamu safi na watu wema.
“Mohamad Shnewer was involved in the Fort Dix plot, the Dukas, (are) good people, were innocent. I still don’t know why the Dukas are in jail.” Mahmoud Omar amenukuliwa akisema.
Bwana Firik Duka na mkewe Lata Duka walihamia Marekani miaka ya mwanzoni mwa 1980s baada ya kusambaratika dola ya Yugoslavia. Wakiwa ni Waislamu kutoka Albania, na wakiwa na watoto wao watatu, walitua na kuanza maisha yao mapya Bensonhurst jirani na Brooklyn, New York. Haukupita muda wakapata watoto wengine wawili, msichana akiitwa Naze na mvulana Burim. Kwa upande mwingine, vijana wao wakubwa, Shain, Tony na Eljvir wakajikuta wakiyavaa maisha ya Kimarekani. Wakauweka kando Uislamu. Sigara, ulevi, miziki, wasichana na mambo kama hayo, ikawa ndio mtindo wa maisha.
Ilitokea siku moja Shain akiwa na rafiki yake wa kike (girl friend) aitwaye Jennifer Marino, walipata ajali ya gari. Japo haikuwa ajali mbaya sana, lakini ikaja kubadili maisha ya kijana huyo. Akikumbukia Uislamu wake akiwa nyumbani kwao Albania, alijiambia:
“Hivi unaweza kufa wakati wowote! Hivi ningekufa katika ajali hii nikiwa na huyu msichana katika gari, ningejitetea vipi mbele ya Mungu wakati nimekufa na kidhibiti.”
Maswali hayo yalimpelekea Shain kubadili maisha. Akaacha kuvuta sigara, pombe, mambo ya wasichana na mengine ya haramu. Swala tao na Msikitini hakosekani. Akawavuta na ndugu zake.
“Nilianza kurejea kuisoma Qur’an na nilijiambia, sitakuwa mnafiki. Siwezi kuswali na kufunga huku naenda ”nightclub” kulewa na wasichana.”
Ilikuwa ni kama kheri ndani ya shari. Vijana katika familia ya Duka wakairejesha furaha ya mama na baba yao ambao walikuwa wakisononeka kuona vijana wao walivyoitupa Dini yao.
“Nilitokwa na machozi kwa furaha waliponiambia kuwa wataanza kuswali,” anasimulia mama yao Bi Lata.
Kule Marekani kuna maeneo maalum ambapo watu huenda kufanya mapumziko au ‘pikiniki’ ambapo ni pamoja na kushiriki michezo mbalimbali ikiwemo mpira, kuteleza katika barafu (skiing), ‘paintball in the woods’, kupanda farasi na kulenga shabaha (shooting range). Wapo watu maalum na silaha mkija mnakodishwa bunduki mnafundishwa kulenga shabaha. Moja ya maeneo hayo ni lile linalojulikana kama Poconos Mountains, Northern Pennsylvania ambapo vijana hawa wa familia ya Duka nao walikwenda siku moja. Hiyo ilikuwa ni Januari 2006.
Wakiwa vijana wa Kiislamu, kila walipokuwa wakipiga shabaha na kupatia, walikuwa wakipiga Takbir na kusema “Allahu Akbar”. Aidha walikuwa na kamera ambapo walikuwa wakipiga picha za video michezo yote waliyokuwa wakifanya.
Wakiwa hawajui hili wala lile, kumbe ile kuonekana vijana wenye devu, wanafanya mchezo wa kulenga shabaha na michezo mingine (jambo ambalo ni la kawaida) huku wakipiga takbiira, ilipelekea taarifa zao kufikishwa kwa makachero wa FBI. Kule walipokwenda kuhariri na kufanya nakala ili kila mmoja wao apate nakala yake, nakala ya CD/DVD hiyo ikachukuliwa na kupelekwa FBI wao wakiwa hawana habari.
Baada ya kuipata CD hiyo mwaka huo huo wa 2006, FBI wakamwendea Mahmoud Omar na kumpa kazi. Huyu Mahmoud Omar, mzaliwa wa Misri, alihamia Marekani mwaka 1990 na akawa anafanya kazi ya kununua magari na kwenda kuyauza Misri. Hata hivyo alikuwa akikabiliwa na tuhuma kuwa baadhi ya magari aliyokuwa akisafirisha yalikuwa ya wizi. Kwa hiyo alikuwa ameingia katika ‘buku jeusi’ la FBI. Katika hali hiyo, ikawa rahisi kwa FBI kumpa kazi, kwa maana kuwa awafanyie kazi ili nao wasimwandame kwa tuhuma zinazomkabili. Alichotakiwa kufanya Omar ni kuwafuatilia vijana wale (na kuwatia katika hatia ya ugaidi).
Alipewa picha ya mtu mmoja akiitwa Mohamad Shnewer. Huyu Shnewer alikuwa rafiki wa karibu wa familia ya Duka na baadae akaja kuwa shemejie Eljivir (dada yake aliolewa na huyu Eljivir). Kwa maelekezo ya FBI ilionekana kuwa Omar asingeweza kuwanasa ‘Duka brothers’ ila kwa kupitia mtu wa kati waliyemwamini. Na ukisoma kisa hiki, utakuja kugundua kuwa FBI walikuwa wamefanya kazi yao vizuri. Walimjua huyu Mohammed Shnewer kuwa ni mchemkaji, mhemkwaji, rahisi kumnasa.
Kwa ufundi mkubwa, Mahmoud Omar akajenga urafiki na Shnewer kama Muislamu mwenzake, wakiswali pamoja msikiti mmoja. Kidogo kidogo Omar akaanza kuleta ‘stori’ za Afghanistan, Iraki na jinsi Majeshi ya Marekani yanavyouwa Waislamu katika nchi hizo. Alipoona kuwa Shnewer ameguswa na habari zake, akaenda hatua ya pili. Ilipofika August 2006, akajenga hoja. Vipi wao kama Waislamu wasifanye kitu kuwatia japo jeraha ‘makafiri’ wanaomwaga damu ya Waislamu! Japo hawawezi kwenda Iraq, basi wawafanyizie hata hapo ndani ya Marekani na bora kulenga wanajeshi kwa sababu ndio wanakwenda kupigana na kuuwa Waislamu Iraq na Afghanistan.
Katika mazungumzo hayo, Mahmoud Omar akachagua Kambi ya Kijeshi iliyo jirani kuwa ndiyo wanayoweza kufanya shambulizi, hata kama watauliwa potelea mbali, wapo katika Jihad. Kambi hiyo ni Fort Dix military base, jirani na Trenton, New Jersey. Mahmoud Omar, akafanya kila njia akapa ramani ya Kambi hiyo ya kijeshi. Alipohakikisha kuwa Shnewer ameshanasa kisawasawa katika mtego, akaja na hoja.
“Unajua kazi hii hatuwezi kuifanya sisi wawili peke yetu, tunahitaji watu zaidi, lakini wawe watu wa kuaminika. Watu unaowaamini, Waislamu safi, sio wanafiki.”
Alisema Omar akimshawishi Mohammed Shnewer kutafuta washirika wengine. Hapo ndio Shnewer akaja na wazo la kuwahusisha ‘Dukas’, yaani vijana ndugu Eljvir Duka,Tony na Shain. Zoezi lilikuwa gumu na lililochukua muda mrefu. Mwisho wa yote, Omar hakufaulu. Vijana japo hawakujua kuwa wametegwa, lakini walikuwa wakitumia tu akili ya kawaida. Walimwambia Omar na rafiki yao Mohammed Shnewer kuwa wao Jihad kubwa wanayoiona na yenye tija katika mazingira wanamoishi, ni kupambana na nafsi zao waweze kuishi Kiislamu katika mazingira yale ya kikafiri. Aliwahi kusema Profesa Omar Hassan Kasule kuwa huku Dar es Salaam na Kampala, tunamsikia tu shetani, lakini ukiwa Washington (Marekani), unakutana na shetani barabarani na mitaani. Unamuona waziwazi shetani kwa jicho. Alichokuwa amemaanisha ni kuwa maasi ya kila sampuli yametapakaa na huru kufanyika kiasi kwamba kunusurika, yahitaji Jihad kubwa ya nafsi. Huo ulikuwa ndio msimamo wa vijana hao.
Lakini wakaongeza kuwaambia rafiki zao kuwa Jihad ya pili na yenye manufaa, ni kuhakikisha familia zao zinaishi Kiislamu. Kisha wafanye Da’wah kuhakikisha kuwa wasio Waislamu katika Marekani, wanaujua Uislamu. Asije akabakia hata Mmarekani mmoja wa kutoa hoja mbele ya Mungu siku ya Kiama kuwa hakufikiwa na ujumbe. Hiyo ndio busara na hayo ndio ya kufanya. Sio kweda kurusha risasi katika kambi ya jeshi ukauliwa ukidhani utakwenda Peponi.
Kila Mahmoud Omar alipokuwa akikutana na vijana hawa, kazi yake kubwa ilikuwa kupenyeza maneno na maswali ili wajibu namna anavyotaka, maneno yao yaje kuwa ushahidi wa kuwatia hatiani. Anaweza kuuliza kwa mfano, unaonaje, Jihad ikianza hapa Marekani utashiriki? Unawaonaje wale askari wa Marekani wanaouwa Waislamu Iraq, je, sio halali kuwauwa ukipata fursa?
Lakini pia alikuwa akiwajia na mikanda ya video ikionesha mapambano Iraq, Afghanistan na mingine ikidaiwa kuwa ni Waislamu wakifanya mazoezi ya Jihad. Ile kwamba walishiriki kuitizama, ilichukuliwa kwamba walipenda na huo ukawa moja ya ushahidi uliowatia hatiani.
FBI walipoona kuwa Omar anashindwa kuwashawishi ‘Duka Brothers’ wakubali kushambulia kituo cha kijeshi- Fort Dix military base, wakaona watafute ‘shushushu’ mwingine wa ziada. Safari hii wakachukua mtu ambaye ni kutoka Albania kama wao wakiamini kuwa atakuwa na ushawishi mkubwa kwao kwa vile ni ‘wapoti’ (home boy). Huyu alikuwa Besnik Bakalli. Besnik Bakalli, akiwa na umri wa miaka 29, aliingia Marekani kwa njia za panya akitokea Albania (undocumented immigrant from Albania). Wakati huo alikuwa katika jela moja kule Philadelphia akisubiri kurejeshwa kwao. FBI wakamwendea wakapa kazi kwamba akiifanikisha, hatafukuzwa na atalipwa pesa nyingi.
Wapo rafiki zangu wakishaswali pale msikiti wa Ibadhi au Suni, maeneo ya Kitumbini, jijini Dar es Salaam, hupenda kukutana pale Zahiri hotel kunywa chai na kuongea hili na lile katika habari za mji zikiwemo za kisiasa na kidini. Katika kupewa maelekezo, Bakalli aliambiwa na FBI kuwa ‘Duka brothers’ wakishaswali msikiti wa Palmyra, hasa siku za Ijumaa, hupenda kwenda Dunkin- (Dunkin’ Donuts), Cherry Hill, ambapo huuzwa vitafunwa mbalimbali, juisi, ice creams, chokoleti, bisikuti, kahawa na ‘take aways’ za kila aina.
Ilikuwa ni Ijumaa moja ya mwezi Julai 2006, ambapo vijana hao walipoingia Dunkin’ Donuts , Besnik Bakalli akiwa katangulia kufika hapo, alijifanya anaongea na mtu kwenye simu kwa sauti kubwa kwa lugha ya Kialbania. Vijana wale waliposikia mtu anaongea lugha ya kwao, wakaingia shauku. Wakamsubiri akamaliza kuongea, wakamsogelea, wakamsalimia na kujitambulisha. Habari ni ndefu kidogo, lakini ufupi wa maneno yule bwana alifanikiwa kujifanya hana mahali pa kukaa akakaribishwa akawa mmoja wa familia ya Dukas. Akapewa kazi katika moja ya miradi yao.
Kama mwenzake Omar, baada ya muda akaanza na mada za kuonea uchungu Waislamu wanaoteswa Afghanistan na Iraq na kwamba itakuwa ni unafiki na ukafiri kama Waislamu hawatashika silaha kupambana. Vijana wale walikuwa wakimhurumia tu Bakalli wakimuona ni mtu mwenye uchungu na dini yake lakini ama mjinga au mwenye uoni finyu. Wakimwambia wewe mwenyewe hapa umefadhiliwa, Waislamu Marekani yote kiduchu, kama tone la maji katika bahari. Unapambana na nani?
“We can’t … we … the biggest Jihad for us here in America is to spread Islam … That’s the most important thing. That is war, believe me. That is Jihad. Jihad is not just, like we say, to go fight. No people misunderstand it. … The first Jihad is with yourself, when the devil tells you, do this, you try, you fight with the devil. No, no, no. I won’t do it. Then the second Jihad is with your family. To work. To teach Islam to your children. Then you should spread Islam in, to tell others, this is Islam. Our biggest obligation for us is our family, especially for me with children.”
Alisema Tony akimjibu Bakalli alipoona anakazana kumtia hamasa na shinikizo waingie msituni wakajifunze silaha ili ‘wafanye jambo’ la kuwatia adabu ‘makafiri’. Ufupi wa maneno ni kuwa hoja ya Tony na wenzake ikawa ile ile kwamba wapiganie kutekeleza Uislamu, kuelimisha familia zao na jamii ya Wamarekani isiyoujua Uislamu. Lakini naye, kama Omar, huyu Bakalli kila akiongea na akina Tony, huleta mazungumzo ambayo, ni kama ilivyokuja katika ile kanuni ya Uislamu kwamba ukikaa mahali ambapo watu wanazifanyia istizai aya na Dini ya Mwenyezi Mungu kwa ujumla, basi utakuwa pamoja nao ikija adhabu.
Mwaka 2006 ulimalizika bila ya mitengo ya ‘mashushushu’ Bakalli na Omar kuwanasa ‘Duka brothers’. Lakini wakati huo huo, vijana hao hawana habari kuwa marafiki zao hao ni makachero wa FBI.
Hawakati tamaa. Mwanzoni kabisa mwa 2007, vijana Eljvir Duka,Tony na Shain wakiwa na marafiki zao Bakalli, Shnewer na Omar pamoja na kundi la vijana wengine, walikwenda tena pikiniki, wenyewe wakiita “boys weekend”. Omar na Bakalli wakanogesha michezo na mara kwa mara wakitamka maneno:
“Hii sawa kabisa na mazoezi ya kijeshi (This is like an army exactly)”.
Anayasema hayo akiwa yupo na Tony, huku kamera zikirekodi. Hiyo nayo baadae FBI wakayatoa kama ushahidi kuwa vijana hao walikuwa wakifanya mazoezi ya kijeshi kujiandaa na Jihad dhidi ya Marekani.
Omar alipoona kuwa vijana hawavutiki kabisa kufanya shambulio dhidi ya kambi ya jeshi au kituo cha polisi, akaja na mpango mwingine. Kule Albania, kuwa na silaha kama bunduki ni jambo la kawaida na watu hupenda hasa kuwa na bunduki. Na hata Marekani, ilimuradi tu uwe na leseni na kibali. Hata hivyo, kama hujapata uraia wa kudumu kama walivyokuwa ‘Dukas’, huwezi kuruhusiwa kununua silaha.
Mahmoud Omar akaona autumie upenyo huo. Ilipofika March 2007, Omar alimwendea Tony na kumwambia kuwa ana rafiki yake anayeishi Baltimore ambaye anaweza kuwasaidia kupata silaha halafu hapo baadae watakapo kamilisha nyaraka zao za kupata uraia, ‘watazihalalisha’. Lakini kabla ya kuwapeleka kwa muuza silaha, aliongea nao huku akiwauliza maswali ilimuradi tu apate kuwarekodi wakisema kuwa wanataka kununua silaha kwa njia ya magendo.
Ilipofika Mei 7, 2007, Tony na Shain walikutana na Omar katika nyumba moja (apartment), ambapo Omar alidai kuwa ndipo anapoishi. Kumbe ‘apartment’ ile ilikuwa imekodiwa na FBI kwa mwezi ule kwa kazi hiyo tu. Walipofika Omar akawapa orodha ya silaha zinazopatikana na ile ramani ya kambi ya jeshi Fort Dix military base, ikawa ipo ndani ya nyumba hiyo.
Hata hivyo, vijana wale wakashtuka na kushangaa kuona kuwa orodha hiyo ya silaha waliyopewa na Mahmoud Omar, pamoja na kuwa na bunduki za kawaida walizokuwa wakitaka, wakakuta kuna silaha nzito nzito za kijeshi kama AK-47s, handguns, M16 rifles, rocket-propelled grenade launcher — ambayo ni makombora yanayotumika kupigia vifaru na magari mazito ya kijeshi. Katika orodha hiyo kulikuwa pia na M-60 machine gun.
Wakati wanashangaa, ghafla wakavamiwa na FBI na kupelekwa rumande Philadelphia (Philadelphia detention center.) Kijana mwingine Eljvir na mdogo wake Burim, walikamatwa siku hiyo hiyo waliporejea nyumbani (wao hawakuwa ‘nyumbani’ kwa Omar). Ila Burim aliachiwa kwa vile bado alikuwa mdogo na hakuwa ameshirikishwa sana katika mtego.
Wakiwa rumande, Eljvir, Shain na Tony, hawakuwa wakiamini kinachotokea. Wakawa wanajipa moyo kwamba huenda wamekamatwa kimakosa. Labda kuna watu wengine walikuwa wakitafutwa, na punde tu wataachiwa.
Hata hivyo, kesho yake Mei 8, 2007 Mwanasheri Mkuu wa New Jersey, Chris Christie, akaitisha mkutano na wandishi wa habari na kutangaza kuwa wamefanikiwa kukamata watu watatu ambao walikuwa wanajiandaa kufanya Jihad dhidi ya Marekani. Na kwamba katika Jihad hiyo walikuwa wamepanga kushambulia kambi ya kijeshi ya Fort Dix military base ambapo wangeuwa askari, wanawake na askari wanaume wa Marekani.
“Fortunately, law enforcement in New Jersey was here to stop them.”
Alisema Christie akimaanisha kuwa vyombo vya dola vilifanikiwa kuwanasa ‘Mujahidina’ na ‘magaidi’ hao kabla hawajaleta madhara.
Ilikuwa ni mshangao na kupigwa na butwaa, vijana hao walipokuja kubaini wakiwa kizimbani kuwa kumbe rafiki zao wa karibu Mahmoud Omar na Bakalli walikuwa ‘mashushushu’ wa FBI waliotumwa kuwatosa.
Kesi ikanguruma Tony na Shain wakahukumiwa kifungo cha maisha na kuongezewa miaka mingine 30. Kwamba, wakimaliza kifungo cha maisha (?), watumikie tena miaka mingine 30 kwa kosa la kutaka kununua silaha kwa magendo za kufanyia Jihad. Eljvir, yeye akabaki na kifungo cha maisha.
Kwa jinsi ilivyovuta masikio ya vyombo ya habari na wananchi wa nchi hiyo kwa ujumla, kesi hiyo kwa vile ilihusisha watu watano, vijana ndugu watatu na marafiki zao wawili, ikapachikwa jina “Fort Dix Five.”
Katika kukamilisha mchezo huu (entrapment) uliowatia jela ‘Duke Brothers’, Mahmoud Omar alilipwa Dola 238,000 wakati Bakalli, alikuwa akilipwa Dola 1,500 kwa wiki kwa muda wote akifanya kazi hiyo. Aidha, ile amri ya kurejeshwa kwao iliondolewa na sasa ni raia huru kuishi Marekani. Ndivyo taarifa za uchunguzi zinavyoeleza.
Nimekieleza kisa hiki kwa urefu (japo nimefupisha na kuacha mengi), kwa sababu kina mengi ya kujifunza. Kwa anayetaka anaweza kurejea: Christie's Conspiracy: The Real Story Behind the Fort Dix Five Terror Plot By Murtaza Hussain and Razan Ghalayini.
Mhariri wa Tanzania Daima amesisitiza juu ya kutowaonea haya watu wanaoshawishi wengine kufanya vitendo vya kigaidi. Nadhani kama tuna nia ya kweli ya kuinusuru nchi yetu isitumbukie walikozama Nigeria na Kenya, kuna haya ya kuwatizama hawa akina Mahmoud Omar na Besnik Bakalli ambao kuna kila dalili kuwa wapo miongoni mwetu.
Kama ni kweli kuna vijana 50 walikutwa porini wakiwa na majambia, kama ni kweli kuna vijana walikamatwa msikitini Kidatu wakiwa na milipuko na bendera za Al-Shabaab pamoja na sare za jeshi, lazima tutafute, nani anawakusanya vijana hawa, anatumwa na nani na kwa lengo gani.
Katika kesi ya James Cromitie (Mmarekani aliyesilimu), ambaye naye alishitakiwa kwa kesi ya ugaidi, katika kutoa hukumu, Jaji Colleen McMahon, aliishutumu serikali kwamba ndiyo iliyomfanya Cromitie kuwa ‘gaidi’. Alisema, Cromitie hakuwa amepanga wala hakuwa na uwezo wa kufanya ugaidi anaodaiwa kupanga kufanya.
“The Government indisputably “manufactured” the crimes of which defendants stand convicted. The Government selected the targets. The Government designed and built the phony ordnance that the defendants planted (or planned to plant) at Government-selected targets. The Government provided every item used in the plot: cameras, cell phones, cars, maps and even a gun. The Government did all the driving (as none of the defendants had a car or a driver’s license). The Government funded the entire project. And the Government, through its agent, offered the defendants large sums of money, contingent on their participation in the heinous scheme.”
Alifafanua na kusema Jaji Colleen McMahon, japo pamoja na hayo yote aliwatia hatiani watuhumiwa (labda kwa kosa la kutokutumia akili na kuona kuwa wanategwa)-Tazama Latest FBI Claim of Disrupted Terror Plot Deserves Much Scrutiny and Skepticism-By Glenn Greenwald and Andrew Fishman.
Anachomaanisha jaji katika maneno yake niliyoyanukuu kama alivyoyasema kwa Kiingereza ni kuwa kama sio mchezo wa FBI, mtuhumiwa asingeweza kufanya hayo yanayodaiwa kuwa ni ugaidi. Akafafanua zaidi akisema kuwa taasisi hiyo na nyingine za kupambana na ugaidi ndio zinabuni uhalifu, kutafuta watu wa kutekeleza na kuwawezesha ikiwa ni pamoja na kutoa magari, silaha na vifaa mbalimbali vya kufanyia kazi.
Katika tasnia ya filamu, kuna kitu kinaitwa ‘movie prop’ au ‘movie property’ na ’movie costumes’, ikiwa na maana ya vitu vinavyotumiwa na mchezaji/msanii wa filamu katika kunogesha uhusika wake. Katika shambulio la Ufaransa, tunaambiwa kuwa polisi walikuta bendera yenye maandishi ya Kiarabu na washambuliaji walikuwa wakisema ‘Allahu Akar’. Katika lile tukio la Turiani, Morogoro ambapo tuliamiwa kuwa kuna vijana walikamatwa msikitini, tuliambiwa pia kuwa ndani ya mabegi yao kulikuwa na bendera nyeusi yenye maandishi ya Kiarabu. Braghashia, kanzu, vilemba, ndevu, nazo ni katika ‘costumes’ ambazo zimekuwa zikipamba uhusika wa matukio kama haya.
Picha inayojitokeza hapa ni kuwa mwandishi wa ‘script’ za tamthilia hizi, ni mmoja. Lakini hata pia mtaalamu wao wa ‘props’ na ‘costumes’, ni huyo huyo mmoja.
chanzo: annuur
Share on Google Plus

About mfaume

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment